11 Februari 2022 - 11:57
Mwanajeshi mfanya mapinduzi ajitangaza Rais nchini Burkina Faso

Mwanajeshi aliyefanya mapinduzi nchini Burkina Fase ametangazwa kuwa Rais wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi mwezi uliopita.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa zinasema kuwa, Baraza la Katiba la Burkina Faso limemtangaza Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, kuwa rais wa nchi hiyo. 

Taarifa ya baraza hilo imesema pia kuwa, Paul-Henri Damiba ndiye amirijeshi mkuu wa majeshi yote ya Burkina Faso hivi sasa.

Tarehe 31 mwezi uliopita wa Januari, wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Burkina Faso walitoa taarifa kuhusu uamuzi huo wa kumtangaza Damiba kuwa rais na kusema kwamba, atakuwa na makamo wawili wa rais.

Baraza la Katiba la Burkina Faso limesema pia katika taarifa yake hiyo kwamba, Damiba ataapishwa rasmi kushika nafasi hiyo, ingawa halikusema jambo hilo litafanyika lini.

Tarehe 24 mwezi uliopita wa Januari, maafisa wa kijeshi wasioridhishwa na uongozi wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Roch Marc Christian Kabore, ambaye alichaguliwa kwa kura za wananchi, walifanya mapinduzi na kutwaa madaraka kwa nguvu.

Wapinzani waliwaunga mkono wananjeshi baada ya kutokea mapinduzi hayo wakisema kuwa Kabore ameshindwa kulinda usalama wa nchi mbele ya magenge ya kigaidi.

Wiki iliyopita wanajeshi hao waliofanya mapinduzi nchini Burkina Faso waliruhusu kuendelea mchakato wa katiba na waliondoa marufuku ya kutotembea usiku ili kukwepa mashinikizo ya nchi nyingine za magharibi mwa Afrika.

Tarehe 24 mwezi uliopita, wanajeshi hao waliahidi kurejesha utawala wa katiba ingawa hawakusema hilo litafanyika lini. Walisema tu watarejesha utawala wa katiba katika wakati unaofaa.

342/